Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Maji

Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Igunga
(IGUWASA)

Mkataba wa Huduma kwa Wateja

Mkataba huu wa Huduma kwa Mteja ni ahadi na makubaliano ya kimaandishi kati ya Mamlaka ya Majisafi, wadau pamoja na wateja wetu. Aidha, mkataba huu unataja masuala mbalimbali yanayohusu aina za huduma zinazotolewa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Igunga (IGUWASA), ubora wake na viwango ambavyo tunaamini vitakidhi mahitaji na matarajio ya wadau na wateja wetu. Aidha, unaainisha maadili ya watumishi, haki ya mteja wa Mamlaka na wajibu wao ili wapate huduma bora kulingana na matarajio yao. Lengo la kuwa na mkataba huu ni kuhakikisha kuwa Mamlaka ya Maji inatoa huduma sahihi, bora na kwa wakati.

Mkataba huu pia unaeleza jinsi wateja na wadau watakavyotoa maoni na malalamiko kuhusu huduma zote zinazotolewa na taratibu za rufaa endapo hawataridhika na huduma hizo. Wateja na wadau wetu watashirikishwa wakati wa kuhuisha mkataba huu kila baada ya miaka mitatu au kila mabadiliko muhimu yanapotokea kwa nia ya kutathimini utekelezaji wa majukumu yetu. Tunaamini kuwa, hatua hiyo itatusaidia kwa pamoja kubaini ufanisi katika utoaji huduma, mafanikio na changamoto zinazotukabili katika kutekeleza majukumu ya Mamlaka ya Maji.

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira inatoa huduma ya Maji kata ya Igunga na maeneo ya pembezoni mwa Mji wa Igunga ikiwemo kata ya Mbutu, Kata ya Isakamaliwa katika kijiji cha Hindishi, Kata ya Nguvumoja katika kijiji cha Mwalala na Kata ya Mwamashimba.

Chapisho hili ni kusaidia IGUWASA kutambua matarajio ya wateja ili kuinua viwango vya huduma kila wakati, mambo mbalimbali yataelezwa ndani ya chapisho hili ikiwa ni pamoja na madhumuni ya chapisho, maelezo, mawasiliano na wateja, viwango vya huduma vinavyotolewa kwa wateja, haki na wajibu wa mteja, mwitikio na malalamiko ya wateja na mapitio ya mkataba.

Mwisho, tunaamini kuwa, tutapata ushirikiano mzuri kutoka kwa wateja na wadau wetu katika kutimiza azma ya mkataba huu, ili kuimarisha mahusiano mazuri katika utendaji na utoaji huduma na kuleta mafanikio katika sekta pamoja na Taifa kwa ujumla. Tunashauri wateja na wadau wetu, kuufahamu kwa kina na ufasaha mkataba huu na kuutumia ipasavyo.